Tuesday 4 April 2017

ZITTO AMPA TANO RAIS MAGUFULI KWA MARA YA KWANZA



Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amefunguka na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuanza kuthamini mchango wa watu ambao wako nje ya CCM na kuwajumuisha katika serikali yake kwa lengo la kuisaidia nchi  katika mambo ya maendeleo.

Zitto Kabwe amesema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa wananchi juu ya chama chake cha ACT Wazalendo kukubaliana na barua ya kujiuzulu nafasi ya mshauri wa chama aliyoandika Profesa. Kitila Mkumbo baada ya kuteuliwa na Rais kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

"Uteuzi wa Profesa. Kitila Mkumbo unaonesha ndani ya vyama vya upinzani kuna watanzania, wenye uwezo, ueledi, na uzalendo wa kuweza kutumika katika utumishi wa umma, na kama unafahamu kuwa Profesa. Kitila Mkumbo ni mtumishi wa umma, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa hiyo nafasi hii ni kupanda cheo tu ndani ya utumishi wa umma". Amesema Zitto.

Mbali na hilo Zitto Kabwe alikwenda mbali na kusema kitendo cha Rais kumteua Profesa. Kitila Mkumbo ni ishara kuwa Rais ameanza kuona kuna watu wengine bora nje ya Chama Cha Mapinduzi. 

"Rais aliwahi kutamka huko nyuma kwamba katika serikali yake hawezi kuteua watu kutoka vyama vingine tofauti na Chama Cha Mapinduzi, kwa hiyo hili linaonesha kuwa wapo watu nje ya Chama Cha Mapinduzi ambao wana uwezo wa kuitumikia nchi" alisema Zitto Kabwe  .

Pia Zitto amesema chama hicho kinamtaka Kitila kwenda kufanya kazi kwa uwezo wake wote kuhakikisha kuwa kero ya maji inatatuliwa, huku akijibu hisia za baadhi ya watu wanaouzungumzia uteuzi huo kwa mitazamo tofauti

"Kuna watu wanaliona hili kama njia ya kuipoza ACT baada ya kukosa nafasi ya uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki, lakini kuna wengine wanaliona kama njia ya kuudhoofisha upinzani kwa kuua nguvu za chama cha ACT Wazalendo, lakini sisi msimamo wetu ni nchi kwanza, tumeona tutangulize maslahi ya nchi badala ya maslahi ya chama, na ndiyo maana tumekubali" Alisema Zitto akijibu maswali ya waandishi.

Kuhusu Kitila kuachia nafasi yake ndani ya chama, Zitto amesema "Kwa nafasi hii ya Ukatibu Mkuu ndugu Kitila hawezi kuendelea tena kuwa mshauri wa chama, kwa hivyo ameandika barua ya kujiuzulu mimi nimeipokea barua yake na nimekubalina naye" alisema Zitto Kabwe.


No comments:

Post a Comment