Dar/Sumbawanga. Mfanyabiashara Mohammed Mohammed (46), mkazi wa Boko Chama jijini Dar es Salaam amemuua mkewe Sophia (36) kisha kujiua akiacha ujumbe wenye kurasa 80 uliobeba sababu za kufanya tukio hilo.
Katika ujumbe huo ambao upo katika nakala sita ambazo alielekeza watu wanaopaswa kukabidhiwa, aliomba mtu yeyote asihusishwe na mauaji hayo.
Ametaka nakala hizo zipelekwe Polisi, kwa mwanaye wa kiume anayeishi Masasi, mjomba wake, baba mwenye nyumba, baba mkwe na nyingine kwa majirani.
Katika ujumbe uliomo kwenye waraka huo, Mohamed alieleza kwamba uamuzi huo ulikuwa katika nafsi yake akisema umetokana na mgogoro wa kimapenzi muda mrefu kati yake na mkewe.
Imedaiwa kwamba katika tukio hilo, Mohammed alimpiga mkewe kwa nyundo kichwani, kumchoma kisu ubavuni na kumchinja kwa kutumia kisu kilichoonekana kuwa kipya.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mjumbe wa Shina Namba 2 Mtaa wa Boko Chama Msikitini, Abdallah Kassim alisema marehemu alionekana kupanga kutekeleza tukio hilo kwa muda mrefu kutokana na baadhi ya vitu walivyoona akidokeza kuwa inawezekana maandalizi yake yalifanyika kwa zaidi ya mwezi mzima.
“Tumekuta chumbani kwake barua yenye kurasa nyingi. Ina michoro ya kisu, nyundo na maandishi yameandikwa na kuchorwa kwa kutumia kompyuta jambo ambalo haliwezi kufanyika hata ndani ya wiki moja,” alisema Kassim.
Alisema hata vifaa alivyotumia katika kutekeleza tukio hilo vinaonekana kuwa vipya na vilikuwa vimeandaliwa maalumu kwa kazi hiyo. Shuhuda huyo alisema katika barua hiyo, mume huyo aliandika kuwa mwanamke huyo amekuwa akidai kuwa watoto waliozaa naye siyo wa kwake, huku akimtuhumu kutumia dawa za kishirikina kumfanya kuwa kama mpumbavu na kuchukua fedha zake (mume) na kwenda kujenga kijijini kwao.
Kassim alisema mwishoni mwa ujumbe huo, marehemu Mohammed amewausia wanawake kuwa makini katika maisha yao ya ndoa na wasipende kuwa na marafiki wanafiki.
Mwenye nyumba waliyokuwa wakiishi marehemu hao, Mwinyi Ramadhani alisema Mohammed alikuwa mtulivu asiyependa makundi na hata siku moja hawajawahi kusikia akigombana na mkewe na kwamba tukio hilo limewashangaza.
“Mohammed ameishi katika nyumba yangu zaidi ya miaka mitatu. Hata siku moja sijawahi kusikia akigombana na mkewe wala kupokea kesi yoyote kutoka kwake au wapangaji wenzake wakimshtaki. Mambo yake alikuwa akimaliza mwenyewe,” alisema Ramadhani.
Hata hivyo, alisema marehemu Mohammed ambaye ameacha watoto wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume ambao wamechukuliwa na ndugu, alikuwa mtu wa kulalamika kuwa wanawake ni watu wenye matatizo lakini hakuwa mtu wa kuhitaji msaada wa mawazo kwa wengine.
Mpangaji mwenzake, Helen Zacharia alisema walikuwa wakiishi vizuri na marehemu Sophia na mumewe na hakuwahi kuwasikia wakilalamika juu ya kutokuelewana.
“Kwa jinsi walivyokuwa wakiishi, hatukuwahi kuwaza kama kitu kama hiki kitaweza kutokea kwani hatukuwahi kusikia hata siku moja wakigombana,” alisema.
Michael Robert ambaye alijitambulisha kuwa ni mdogo wa marehemu Mohammed, alisema kuwa wameelezwa na polisi kuwa uchunguzi wa suala hilo haujakamilika na kwamba leo watapata kauli ya jeshi hilo kauli ambayo ilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda ambaye alisema upelelezi unaendelea ili kujiridhisha kama ni kweli marehemu Mohamed ndiye aliyetekeleza tukio hilo.
Watatu wa familia moja wauawa
Wakati mauaji hayo yakitokea Dar es Salaam, watu watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Kipa, Sumbawanga wameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana kwa tuhuma za ushirikina.
Tukio hilo lilitokea Jumatano iliyopita saa 2:45 usiku katika Kijiji cha Mfinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando aliwataja waliouawa kuwa ni Joachim Kayanda (60), Everina Mwanakatwe (47) na Emmanuel Kayanda (27) ambao imeelezwa kwamba walikwenda Mfinga kwa shughuli za kilimo.
Kamanda Kyando alisema wanafamilia hao waliuawa walipokuwa wakijiandaa kulala ambako kundi la watu lilivunja mlango na kuwavamia likiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Alisema watu watano wanahojiwa kutokana na mauaji hayo na alitoa rai kwa wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji ya kujichulia sheria mkononi mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment