Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemzuia shahidi wa kwanza
katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na
wenzake watatu, kujibu swali linalohusu mamlaka ya kikatiba ya
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi
uliofanyika Oktoba 25,2015. Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba , swali hilo la Lissu halina mashiko.
Lissu
alimuuliza shahidi ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Ilala,
Salum Hamduni kwamba, Jecha Salim Jecha ana mamlaka gani kikatiba kufuta
uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Lissu
alimuuliza Kamanda Hamduni kama anafahamu mamlaka yapi ya kikatiba
ambayo Mwenyekiti wa ZEC, Jecha aliyatumia kufuta uchaguzi mkuu wa
madiwani, wabunge na Rais.
Wakili
wa Serikali, Paul Kadushi amedai kuwa shahidi huyo amekwenda mahakamani
kutoa ushahidi kuhusu maelezo na kwamba si kutoa tafsiri ya kisheria
kuhusu Katiba ya Zanzibar.
Kadushi
amedai anapinga shahidi wake kujibu swali hilo kwamba Mwenyekiti wa ZEC
ana mamlaka ya kufuta uchaguzi ama la na kueleza kuwa shahidi huyo hana
ufahamu wa sheria na si mtaalamu wa Katiba na sheria.
''Napinga
shahidi kujibu swali hili ambalo kimsingi linamtaka atafsiri sheria,
jambo ambalo silo lililomleta na wala hana utaalamu wa kisheria. Hata
hivyo, mahakama hii haina mamlaka ya kutafsiri Katiba isipokuwa ni
mahakama ya kikatiba na mahakama kuu ndio yenye uwezo huo,'' alidai Kadushi.
Lissu
alipinga hoja hizo kwa maelezo kwamba, pingamizi la wakili wa serikali
halina maana kwa sababu suala la mamlaka halali au si halali ya Zanzibar
limeletwa na upande wa mashitaka wenyewe, kama ambavyo mashitaka ya
pili katika kesi hiyo wameeleza kuwa habari iliyochapishwa ingeweze
kuleta chuki kwa Wazanzibar kuichukia nchi yao.
Alidai
kuwa, masuala ya mamlaka wameyaleta wenyewe wanapaswa kukabiliana nayo,
kwa kuwa Sheria ya Ushahidi namba 147, kifungu kidogo cha pili na
Sheria namba 157 ya sheria hiyo, vinaweka wazi kwamba shahidi anaweza
kuulizwa swali lolote na kwamba si lazima liwe ndani ya kile
anachokitolea ushahidi.
Hakimu Simba amesema, mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuzungumzia Katiba ya Zanzibar.
Amesema
mahakama katika kesi hiyo haitazungumzia uhalali au kutokuwa halali kwa
Mwenyekiti wa ZEC, Salim Jecha kufuta au kutofuta uchaguzi mkuu
Zanzibar.
"Pingamizi
la upande wa mashitaka ambao ulipinga masuala ya kikatiba ambayo mbunge
huyo alikuwa akimuuliza shahidi kuhusu Jecha ana mamlaka gani kikatiba
kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015, ni sahihi na shahidi
hatakiwi kujibu swali hilo," amesema Hakimu Simba.
Lissu
amedai uamuzi huo hautamuathiri na kwamba anakubaliana nao kwamba
haruhusiwi kuuliza swali hilo kwa shahidi hivyo waendelee na ushahidi.
Hakimu
Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 8 na 9, mwaka huu na kuutaka
upande wa mashitaka kupeleka mashahidi ili kesi iishe kwa kuwa watu
wengi wanaifuatilia hivyo iishe waendelee na shughuli za maendeleo.
Washitakiwa
wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina,
mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya
Jamana, Ismail Mehboob.
Wanadaiwa
kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa lengo la kuleta
chuki kwa wananchi wa Zanzibar, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja
waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari
kisemacho, 'Machafuko yaja Zanzibar'.
Katika
mashitaka yanayomkabili Mehboob, anadaiwa kuwa, Januari 13 katika jengo
la Jamana, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na
taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha
hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
No comments:
Post a Comment