Tuesday, 7 March 2017

Pamoja na Kuachiwa ,Polisi Waing'ang'ania Simu ya Lissu..!!!!


MNADHIMU wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, juzi alikamatwa na polisi na kushikiliwa kwa saa kadhaa kisha kuachiwa kwa dhamana huku simu yake ikibaki polisi kwa kile kilichodaiwa ni kwa upelelezi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro, alivyotafutwa kueleza sababu za kubaki na simu hiyo, alijibu kwa kifupi: “Sababu za upelelezi siwezi kusema.”
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema kwamba simu ya Lissu iliyobaki polisi ni aliyoitumia kutuma ujumbe mfupi uliosambaa katika makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii ikielezea kukamatwa kwake akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
 “Walimkamata kuhusu mambo aliyotamka huko Zanzibar kwenye mkutano wa hadhara,  sasa sijui kwanini wabaki na simu yake, eti wanasema ni kwa ajili ya uchunguzi, sasa huo uchunguzi wa matamko ya kwenye mkutano wa hadhara na simu sijui vinaingilianaje,” alisema.
Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alisema Lissu aliachiwa kwa dhamana ya polisi iliyowekwa na wanasheria Hekima Mwasipu na Nashon Nkungu kwa sharti la kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Machi 13.
Makene alisema kuwa Lissu alikamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi ambayo yangeweza kuibua mtafaruku wa kidini katika jamii, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Bimani, Zanzibar, Junuari mwaka huu.
Juzi muda mfupi baada ya kukamatwa, Lissu alituma ujumbe ambao pamoja na mambo mengine ulisema: “Kwa wananchi wote wa Tanzania. Nimekamatwa tena. Nimekamatiwa mahakamani Kisutu mara tu baada ya waendesha mashtaka wa Serikali hii kunifutia kesi iliyotokana na kukamatwa kwangu bungeni Dodoma mwezi uliopita.
“Hiyo kesi wameifuta kwa maelezo kwamba Serikali haina nia tena ya kuendelea na kesi hiyo. Sikutoka hata nje ya mahakama nikakamatwa tena.
“Wamenileta Central (Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam) kwa mahojiano. Mapolisi walionikamata wamekataa kuniambia wananikamata kwa kosa gani. Kwahiyo sijui kosa nilofanya hadi sasa.
“Nadhani sababu ina uhusiano wa moja kwa moja na Uchaguzi wa Rais wa TLS (Chama cha Wanasheria wa Tanganyika) unaofanyika wiki ijayo. Serikali hii, kwa kutumia mawakili wao vibaraka, imekuwa na mkakati mkubwa wa kunizuia kugombea urais wa TLS.
“Walikuwa wanapanga kwenda kupinga kugombea kwangu mahakamani. Tumewasema hadharani na kuzianika njama zao. Sasa wameamua kutumia rungu lao la siku zote: Jeshi la Polisi.
“Hofu yao ni kubwa sana. Natabiri watataka kuniweka ndani hadi baada ya uchaguzi huo wa wiki ijayo. Natabiri mawakili vibaraka wao wataleta hoja kwenye TLS kwamba mgombea asiyekuwapo ukumbini wakati wa uchaguzi aondolewe kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Nawataka mawakili wanaotaka mwanzo mpya katika TLS wasikubali njama hizi. Hakuna makatazo yoyote katika kanuni za uchaguzi yanayozuia mgombea aliyeteuliwa kuondolewa kwenye uchaguzi kwa sababu tu hayupo ukumbini.
“ Nawaomba washikilie msimamo kwamba wote walioteuliwa kugombea wapigiwe kura na wanachama wa TLS. Iwe mwanzo wa TLS kutimiza wajibu wake kwa wanachama wake na kwa Watanzania. Nimekamatwa asubuhi na mapema. Hakuna sababu ya kutokunipeleka mahakamani leo hii hii.
“Kama hawatanipeleka mahakamani nawataarifu kwamba nitaanza mgomo wa kula chakula na sitakula chakula hadi hapo nitakapopelekwa mahakamani.” ulisema sehemu ya ujumbe huo
MASHA AIBUKA
Baada ya taarifa ya kukamatwa kwa Lissu, mwanasheria wa kujitegemea, Lawrence Masha, aliandika katika mitandao ya kijamii kwamba tabia ya polisi ya kukamata watu baada ya kuachiwa na mahakama au kufutiwa kesi na waendesha mashtaka imeanza kuwa mazoea, hiyo si mara ya kwanza kufanyika.
“Natoa rai kwa watumishi wa vyombo vya dola kwamba waheshimu haki za binadamu na waheshimu misingi ya sheria zetu, kupindisha sheria ili kutimiza malengo ya watu fulani bila kuzingatia misingi ya haki, itatupeleka pabaya kama nchi,” alisema Masha.
ALIVYOKAMATWA
Juzi Lissu aliachiwa huru mbele ya Hakimu Mkazi Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi na kukamatwa tena akiwa katika eneo la mahakama hiyo kisha kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Paulo Kadushi, alidai mahakamani kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewasilisha hati ya kuondoa kesi, hivyo aliomba mshtakiwa aachiwe huru.
Kadushi aliwasilisha hati hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kuonyesha kwamba DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Hakimu Shahidi alikubali na mahakama ilimwachia huru mshtakiwa.
Baada ya kutoka katika chumba cha mahakama, Lissu alikutana na askari waliovalia kiraia, wakamwambia yuko chini ya ulinzi akapande gari la polisi waende kituoni.
KESI ILIYOONDOLEWA
Katika kesi iliyoondolewa, Lissu anadaiwa  Januari 11, mwaka huu maeneo ya Kibunju Maungoni, Mjini Magharibi, Zanzibar katika kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Dimani, alitoa maneno ya ushawishi kwamba tangu mwaka 1964 Tanganyika ndiyo inayoamua nani atawale Zanzibar.
Katika shtaka la pili, alidaiwa kuwa katika tarehe na mahali hapo hapo alisema ‘tangu mwaka 1964 Zanzibar inakaliwa kijeshi na Tanganyika, nani anayebisha… Tangu mwaka 1995 ikifika uchaguzi askari wa Tanganyika wanahamia Zanzibar ili kuja kuhakikisha vibaraka wao wa Zanzibar hawaondolewi madarakani na wananchi mnapigwa’.
Alidaiwa pia kuwaa alisema ‘wananchi mnateswa, mnauawa kwa sababu ya ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar… Marehemu Karume alipoanza kushtuka mwaka 71, 72 akauawa… itakapofikia tarehe 15 mwezi wa kwanza muadhimishe miaka 53 ya kukaliwa kijeshi na Tanganyika’.
Katika shtaka la tatu alidaiwa kusema ‘Jumbe aliondolewa Dodoma na Ally Hassan Mwinyi alipewa urais wa Zanzibar Dodoma na aliyempa ni Nyerere na sio Wazanzibari…marais wa Zanzibar wote ni made in Tanganyika …wametengezwa na Tanganyika , wako madarakani kwa sababu ya Tanganyika’.
Ilidaiwa maneno hayo yalikuwa kwa ajili ya kushawishi watu wasiridhike na wawe na nia ovu.
Lissu akijibu mashtaka alidai “maneno nilisema, lakini kusema kweli si jinai kwa hiyo jibu langu hapana. Ni kweli jeshi tangu lilipoingia Zanzibar mwaka 1964 halijaondoka mpaka sasa, ni kweli Jumbe aliondolewa Dodoma na Ally Hassan Mwinyi aliteuliwa katika kikao hicho hicho mwaka 1984.
‘Hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa inaongozwa na Jaji Joseph Warioba ilisema Tanganyika imevaa joho la Tanzania, hivyo kusema si ajabu wala si kosa, jibu langu hapana.”


No comments:

Post a Comment