Shigongo ni mmoja wa waandaji wakubwa wa matamasha kupitia ukumbi wake wa Dar Live na huenda miaka ya hivi karibuni ameshindwa kuzimudu gharama za kumchukua kutumbuiza. Kupitia Instagram, haya ndio mambo aliyoandika:
Kama nilivyosema wakati naanza kwamba ninampenda sana Diamond kwa sababu amekuwa mtu wa kujituma, aliyeng’ang’ania kutoka kwenye umasikini mpaka kuwa na mafanikio aliyokuwa nayo. Ieleweke kwamba sipo kwa ajili ya kumsema, kumponda, hapana, nipo kwa ajili ya kumshauri kama mdogo wangu, rafiki yangu kwa hiyo naomba nisieleweke vibaya.
Diamond Platnumz kwao ni Tanzania, ni mwanamuziki wa Kitanzania na hata wapenzi wake wengi wanaomsapoti kwa nguvu nyingi ni Watanzania ambao asilimia kubwa vipato vyao ni vya chini mno. Wengi wanatamani kumuona akifanya shoo katika ardhi yake ya nyumbani, lakini badala yake wamekuwa wakimuona mara nyingi akifanya shoo Marekani, Ulaya, Nigeria, Afrika Kusini, kwenye Mashindano ya Afcon na sehemu nyingine nyingi ambazo ni nje ya Tanzania, mahali alipozaliwa na kuthaminiwa, mahali ambapo aliweza kujijazia mashabiki wengi.
Mashabiki zake wanahitaji shoo, kumsoma kwamba amejenga nyumba, amenunua au amepata watoto na Zari si kitu ambacho mashabiki wanakihitaji zaidi kutoka kwake, wanachohitaji ni kuona shoo zake kwa wingi kama kilivyokuwa kipindi cha Moyo Wangu, Kamwambie na nyimbo nyingine.
Ni kweli ana jina kubwa, ana mashabiki wengi, amepambana sana kufika alipokuwa lakini kwa upande mwingine anatakiwa kuangalia gharama za shoo zake hasa anapofanya nchini Tanzania, kwa watu ambao walimfanya leo kujulikana zaidi kama Diamond na si Naseeb Abdul. Leo, Diamond anafanya shoo kwa dola 55,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 100. Hii inamaanisha kwamba kwa mtu kama mimi, nikimchukua Diamond kwa gharama hiyo inamaana kwamba nitataka niingize kiasi kikubwa kama faida, kwa hiyo badala ya kufanya shoo Dar Live, Diamond Jubilee au sehemu nyingine, nitaihamishia shoo yangu Mlimani City na kufanya kiingilio cha shilingi elfu hamsini.
Swali la kujiuliza, je, yule bodaboda anayepiga sana nyimbo za Diamond ataweza kuingia kwa kiingilio cha shilingi elfu hamsini? Yule kijana anayatafuta riziki kwa kuingiza nyimbo za Diamond kwenye simu za wateja ataweza kuingia kwa gharama hiyo? Je, yule kijana wa Tandale, Temeke, Mbagala mwenye fulana kubwa iliyoandikwa WCB ataweza kuingia kwa gharama hiyo? Jibu rahisi ni kwamba hatoweza.
Ni lazima afikirie ajue kwamba gharama anazotoza sehemu nyingine ziwe tofauti na Tanzania, au azifanyie gharama hizo kampuni kubwa za mitandao ya simu na vinywaji lakini si mtu binafsi.
Mara nyingi amekuwa akisema huko nje analipwa zaidi ya milioni mia moja, je, ni halali hata kwa Watanzania wenzake waliomfanya kuwa hapo alipo kuwatoza kiasi hicho cha fedha huku huyo anayemchukua akitarajia shoo yake iingiwe na watu wa hali ya chini wenye kiu ya kumuona?
Labda Naseeb Abdul mwenyewe ndiye aliyelazimisha ada hii, kama si yeye bali ni mameneja wake (Salam na Tale) basi wanamshauri vibaya na matokeo yake kutofanya shoo nyumbani kwake (Tanzania) kutamfanya apoteze kupendwa na mashabiki sababu ya umbali alioutengeneza. Ikumbukwe kwamba watu hununua bidhaa ya mtu wanayempenda, mtu akichukiwa na bidhaa zake hususiwa.
Diamond na WCB ni biashara ya Naseeb Abdul, hivyo basi Naseeb Abdul hatakiwi kuthamini sana fedha na kusahau mashabiki zake waliomfanya kuwa hapo alipo. Kifike kipindi awaeleze mameneja wake “HAPANA! TANZANIA NI NYUMBANI NA HAWA NI NDUGU ZANGU”
Basi kama waandaaji watashindwa kumudu gharama zake sababu Naseeb ni mfanyabiashara kama mimi, basi afanye shoo ya kujitolea (Charity show) kama tuliyofanya naye huko Tandale huko Mwanza, Kigoma, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro kwenye viwanja kwa kiingilio cha shilingi 3000 na kisha fedha hizo azipeleke kusaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na hiyo itamfanya kupendwa na mashabiki na kumfanya kwenda juu kimuziki.
TOFAUTI NA HAPA, MBELE YAKE KUNA SHIMO, UKIMYA WAKE BILA SHOO NYUMBANI
No comments:
Post a Comment