Na Saleh Ally
JUNI 22, 1994, beki Andres Escobar wa kikosi cha timu ya taifa, alijifunga wakati timu yake ya taifa ya Colombia ikicheza mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya kikosi cha Marekani ambao walikuwa ni wenyeji.
Mechi hiyo iliisha kwa Colombia kupoteza kwa mabao 2-1, Wacolombia wengi wakiamini ni wakubwa kisoka kuliko Marekani. Hivyo hawakustahili kupoteza mechi hiyo.
Julai 2, 1994 Escobar aliuawa kwa kupigwa risasi nyingi mwilini wakati akitoka kwenye mgahawa mmoja mjini Medellin, moja ya miji inayoaminika kwa kuwa na makundi lukuki ya wauza madawa ya kulevya.
Uchunguzi ulifanikiwa kumnasa Humberto Munoz ambaye alihukumiwa kwenda jela miaka 42 baada ya kukataa katakata kuwataja waliomtuma. Baada ya miaka 11 alikata rufaa na kufanikiwa kutoka jela. Lakini tayari maisha ya beki “mstaarabu” Escobar, yakawa yamedhulumiwa.
Hivi karibuni, beki mwenye jitihada wa Yanga, Andrew Vincent, alijifunga wakati timu yake ya Yanga ikiwa katika mapambano katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao FC.
Mechi iliisha kwa Mbao FC kushinda kwa bao 1-0 na kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho na kama watashinda dhidi ya Simba, basi wataliwakilisha taifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, kulikuwa na tangazo maarufu lililojulikana kwa jina la “Maimuna”. Alikuwa ni dada mmoja aliyepigiwa simu na baada ya kusikia mtu akizungumza Kiingereza, basi yeye aliendelea kujitambulisha tu, “Mimi Maimuna, Naitwa Maimuna”. Aliendelea kusema hivyo hata alipoulizwa jambo jingine.
Hii ilikuwa ni kuonyesha hakuwa akijua jambo lakini alitaka kuonyesha yeye ni mtu anayejua mambo fulani. Jambo zuri kwa Maimuna angeweza kuonyesha kwamba hajui ili apate nafasi ya kujifunza.
Vincent maarufu kama Dante amekuwa akipata wakati mgumu tangu amejifunga katika mechi hiyo iliyopigwa hivi karibuni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Wapo ambao wamekuwa wakimshambulia kwa maneno na hata vitisho. Amelalamika kupokea vitisho na nimeona wapo waliokuwa wakimlaumu na kumuona hafai tena kwa maneno mabaya ya kashfa ambayo hayastahili.
Kwangu wengi wao nawachukulia kama ni akina “Maimuna” wa mchezo wanaoushabikia. Ushauri wangu ni vizuri kujifunza kabla ya kuzungumza maneno.
Mchezo wa soka hautaki hasira, ukiendekeza hasira kama unapenda soka, utaishia kujiumiza moyo na kujipa msongo wa mawazo.
Ili upande mmoja ufanye vizuri, lazima mwingine ukosee na kukosea lazima wakosee watu ambao mjumuiko wao ndiyo unaounda timu. Beki kujifunga si jambo la kwanza kutokea kwa Dante. Anayefuatilia mpira, anayejua mpira atanielewa hapa.
Tumeona akina “Maimuna” wa Colombia, wamedhulumu haki ya uhai wa Escobar. Leo, wanajuta na kujisikia vibaya na wameendelea kuona katika soka watu wakijifunga na maisha yanaendelea bila mtu kudhulumiwa haki yake ya kuishi au haki ya kawaida.
Lakini Dante ni binadamu, makosa yanatokea. Pia, ajabu ipi kubwa beki kujifunga na hasa kama alikuwa akijaribu kuokoa na mazingira ya mpira wenyewe yanaonekana?
Unamkumbuka beki Pierre Issa raia wa Afrika Kusini ambaye alijifunga mfululizo akiichezea timu ya taifa kwenye Kombe la Dunia na aliporudi Marseille ya Ufaransa akajifunga mfululizo mechi mbili?
Kuendelea kumsakama Dante kwa mashabiki wenyewe wa Yanga ni kujishambulia wenyewe na kuonyesha kiasi gani wao ni kina “Maimuna” katika soka na vema wakabadilika na kujifunza.
Wakati Dante alipojifunga, kuna ambaye amehesabu aliokoa mara ngapi? Lakini jiulize, pamoja na hivyo, waliocheza mbele vipi hawakufunga hata bao moja? Kama lawama ndiyo msingi vipi hazijaelekezwa kwao? Au wakati inapigwa krosi kutoka pembeni kwa nini beki wa pembeni hakuizua mpira usifike kati?
Soka ni makosa na kuzibiana makosa na ndiyo njia sahihi ya kutengeneza timu bora. Dante ni sehemu ya timu, alitaka kutimiza wajibu wake akakosea, wenzake wangeweza kurekebisha, bahati mbaya haikuwa hivyo.
Mimi bado ninaamini Dante ni mmoja wa mabeki bora wanaokuja kuwa faida ya Tanzania. Hapaswi kuzozana na wasiojua au wanaotanguliza ushabiki kupindukia.
Anapaswa kuwa mvumilivu na kuwekeza akili yake katika mechi zijazo za Yanga hasa katika Ligi Kuu Bara. Akiendelea kuwatupia macho na kuacha masikio yake wazi kwa ajili yao, watamfelisha.
No comments:
Post a Comment