Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya
kukamatwa kwa jumla watuhumiwa 349 akiwemo 'video queen' Agnes Gerald
maarufu kwa jina la 'Masogange', katika oparesheni ya kuwasaka watu
wanaohusika na dawa za kulevya.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amesema kati ya watuhumiwa hao, wamo
wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wa dawa za kulevya, na kwamba
wataanza kufikishwa mahakamani siku ya kesho, huku mmoja akipandishwa
kizimbani leo.
Pia ametoa taarifa ya kijana mmoja anayedaiwa kusambaza taarifa za
uongo, ambapo amesema kuwa jeshi hilo linamshikilia kijana huyo ambaye
ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23, anayedaiwa kutaja majina ya
viongozi na kuwatuhumu kuwa wanahusika na dawa na dawa za kulevya.
Kuhusu askari 9 waliotuhumiwa kuhusika na dawa hizo, Kamanda Sirro
amesema askari hao wamekabidhiwa kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za
kisheria.
Kamanda Sirro amesema hadi sasa jumla ya kete 612 pamoja na bangi
vimekamatwa na kwamba kuna watu wengine 17 ambao bado jeshi hilo
linawafuatilia na watakuwa mbaroni wakati wowote.
No comments:
Post a Comment