Sunday, 19 February 2017

Wasira, Bulaya vuta nikuvute


MAJAJI watatu wa Mahakama ya Rufani leo wataanza kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) iliyofunguliwa na 'wapambe' wa aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira.


Katika kesi hiyo ya mwaka 2016, walalamikaji ni wapigakura wa jimbo hilo ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe, aliwataja Majaji watakaosikiliza kesi hiyo kuwa ni Salim Mbarouk atakayekuwa Mwenyekiti akisaidiana na Augustine Mwarija na Shaabani Lila.

Kwa mujibu wa Msajili Kabwe, walalamikaji hao katika dai lao wanapinga uamuzi ulitolewa na Mahakama Kuu uliohalalisha ushindi wa Bulaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kabwe alisema rufani hiyo itasikilizwa mfululizo na jopo la majaji hao.

Pia aliwataja wakili wanaotarajiwa kuwakilishia upande wa walalamikaji kuwa ni Costantine Mtalemwa na Yassin Member, ambao kwa niaba ya wateja wanaiomba Mahakama kutengua ushindi wa Bulaya wakidai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Dai lingine lililotajwa ni kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alitangaza matokeo bila Wasira kuwapo; ambayo wanadai hayakuwa sahihi.
Uamuzi wa ushindi wa Bulaya katika Mahakama Kuu, ulitolewa Novemba 18 mwaka jana na Jaji Noel Chocha.


No comments:

Post a Comment