Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekerwa na mifuko ya mbolea ya kiwanda
cha Minjingu kuchapishwa anuani ya Kenya wakati inazalishwa Tanzania na
kumtaka mwekezaji kumuomba radhi Rais.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho,
waandike barua kwa Rais John Magufuli kabla hajamaliza ziara yake
keshokutwa na apate nakala ya barua hiyo.
Alitoa agizo hilo baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo wilaya
ya Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara.
Waziri Mkuu amerejea Babati jana akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa
na ratiba za kitaifa.
“Nilikuja kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii
haikubaliki huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika
inasaidia kutoa mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa
kukuta mifuko ya kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati
mali ghafi inatoka Tanzania,” alisema.
“Ni kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone
anuani ya Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya
TBS. Kwanini Tanzania haionekani? Kwani malighafi iko Kenya?
haiwezekani, ni lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais
Magufuli. Yeye anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi
mnafanya hivyo?”
Akitoa maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Tosky
Hans alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na
makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na
kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi.
No comments:
Post a Comment