HATIMA ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema),
itajulikana Ijumaa wiki hii baada ya shauri hilo kurudishwa Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha kwa utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.
Hatua hiyo imekuja baafa ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa
Tanzania kufuta rufaa mbili za Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), dhidi ya
mbunge huyo juzi mjini hapa.
Mmoja wa mawakili anaomtetea mbunge huyo, Adam Jabir, alisema shauri
hilo litaamuliwa Machi 3, mwaka huu mbele ya Jaji Salma Maghimbi
kutokana na rufaa ya Jamhuri namba 135 ya mwaka jana, inayopinga uamuzi
wa Novemba 11, mwaka jana wa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,
Desderi Kamugisha kumpa Lema haki ya dhamana.
Novemba 11 mwaka jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali Paul Kadushi,
alisimama wakati hakimu huyo akijiandaa kuandika masharti ya dhamana na
kuieleza mahakama hiyo kuwa wameshasajili notisi ya kusudio la kukata
rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa hakimu huyo kumpa Lema dhamana.
Hata hivyo,uamuzi huo wa dhamana haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.
Hakimu Kamugisha alishindwa kuendelea na mahsarti ya dhamana kwa
mshitakiwa huyo ambapo,alikubaliana na upande wa Jamhuri na kusema kuwa
notisi ina hadhi sawa na maombi ya rufaa yaliyowasilishwa Mahakama Kuu
hivyo mwenendo na uamuzi wake utasimama mpaka uamuzi utakapotolewa na
Mahakama Kuu.
Januari 4 mwaka huu, Jaji Maghimbi alitarajiwa kusikiliza na kutoa
uamuzi kuhusiana na dhamana ya Lema ila ilikwama baada ya mawakili wa
Serikali kukata Rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania,kupinga Jaji huyo
kusikiliza rufaa yao wenyewe.
Jaji Magimbi alitarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa iliyowasilishwa na
upande wa Jamhuri wakipinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpa Lema
haki ya dhamana.
Uamuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na wakazi wengi wa jiji la
Arusha,hasa ikizingatiwa mbunge huyo anashikiliwa katika mahabusu ya
Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi mitatu,tangu akamatwe na polisi
nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Novemba 2, mwaka jana.
Aidha uamuzi huo ulikuwa unatarajiwa kutoa tafsiri ya kisheria ya notisi
ya nia ya kukata rufaa iliyowasilishwa na na mawakili hao wa
Jamhuri,notisi iliyosababisha Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi
kutokuendelea na hatua ya kuweka masharti ya dhamana.
Akiahirisha uamuzi huo mahakamani hapo,Jaji huyo alisema kuwa mikono
yake imefungwa na hawezi kusikiliza na kutoa uamuzi kutokana na
mawakili wa Serikali,kusajili nia ya kusudio la kukata rufaa Desemba 30
mwaka jana,katika Masijala ya Mahakama ya Rufaa Tanzania iliyopo mkoani
hapa, kupinga asisikilize rufaa hiyo.
Awali kabla ya mawakili wa serikali kukata rufaa Mahakama ya Rufaa
Tanzania kupinga kusikilizwa kwa rufaa yao Mahakama Kuu, Jaji
Maghimbi,aliwataka mawakili mawakili wa Jamhuri kuwasilisha hoja zao za
rufaa Disemba 29,huku mawakili wa Lema wakitakiwa kujibu hoja hizo
Disemba 30 kabla ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa rufaa hiyo jana.
Lema anakabiliwa na kesi mbili za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John
Magufuli, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kesi namba 440 na 441.
No comments:
Post a Comment