CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Salome Komba ambaye ni mke wa kada
maarufu wa chama hicho, marehemu Kapteni John Komba, kufuatilia malipo
ya mafao ya mumewe kwa uongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT)
ambako ndiko alikokuwa akifanyia kazi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo, ametoa maelekezo hayo
ikiwa ni siku moja tu baada ya Salome kukaririwa akimuomba Mwenyekiti
wa CCM, Rais John Magufuli aingilie kati kumsaidia ili alipwe mafao ya
marehemu mume wake yanayofikia Sh. milioni 75.
Kwa mujibu wa Salome, hadi sasa wakati mumewe akitimiza miaka miwili
tangu afariki dunia, CCM imemlipa Sh. milioni 4.5 tu ikiwa ni sehemu ya
malipo hayo huku akifuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio kupata kiasi
kilichobaki cha Sh. milioni 70.5.
Akizungumza jana kuhusiana na suala hilo, Mpogolo alisema ofisi yao
haiwezi kulizungumzia kwa sababu masuala yanayohusu fedha yanapaswa
kufafanuliwa vyema na uongozi wa kundi lao la TOT ambako Komba alikuwa
akifanya kazi.
“Ukiniuliza mimi chama kinasemaje (kuhusiana na madai ya mke wa Komba),
sidhani kama nitaweza kuzungumzia hilo kwa kuwa ni suala la fedha … na
masuala ya fedha si unajua… yana taratibu zake za kifedha. Aulizwe
Mkurugenzi wa TOT anaweza kusema nini kinaendelea,”alisema Mpogolo.
Jitihada za kumpata Kaimu Mkurugenzi wa TOT, Gasper Tumaini, ili
azungumzie suala hilo hazikufanikiwa jana. Hata hivyo, Tumaini
alikaririwa pia jana akionyesha kufahamu deni hilo.
Komba aliyezaliwa mwaka 1954, alifariki dunia Februari 28, 2015 na
kuzikwa mkoani kwake, Ruvuma. Enzi za uhai wake, Komba alijizolea
umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake katika kutunga na kuimba nyimbo
mbalimbali za kwaya, hasa za kukipigia debe chama chake (CCM) wakati wa
kampeni za uchaguzi.
No comments:
Post a Comment