Thursday, 27 April 2017

Samatta aisaidia Genk kuwania tiketi ya UEFA mwakani


Mchezaji tegemezi katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania na klabu ya KRC Genk, Mbwana Ally Samatta, amesaidia klabu yake ya Genk kutoka na suluhu ya goli 1-1 dhidi ya kikosi cha AS Eupen mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Kehrweg mjini Eupen, ikiwa ni mchezo wa Kundi B kuwania tiketi ya kucheza michuano ya UEFA Europa League mwakani.
Samatta, ambae hivi karibuni amejikuta akipachikwa jina jipya la utani na wapenzi wa soka nchini lijulikanalo kama 255 Champion, amefanikiwa kucheza dakika zote 90 katika mchezo huo uliochezwa Jumatano usiku na timu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, AS Eupen.
Klabu ya Genk ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy dakika za awali za mchezo huo, kabla ya wenyeji kuchomoa kwa mkwaju wa penalti kupitia mchezaji Luis Garcia katika kipindi cha pili.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania Sama Goals alianza katika kikosi hiko baada ya mchezo uliopita wa michuano hiyo kutokea benchi Jumapili ambapo Genk walishinda 6-0 dhidi ya Royal Excel Mouscron, wakiwa nyumbani Uwanja wa Luminus Arena.
Klabu ya Genk inaongoza kundi hilo la B katika mchuano wa kuwania tiketi ya Europa League kwa kuwa jumla ya point 13 ikiwa imecheza mechi Tano huku Mchezaji huyo akiwa ameshatimiza mechi 54 tangu kujiunga na klabu hiyo akitoka katika klabu ya Tp Mazembe ya DRC alikofanikiwa kufunga jumla ya mabao 18.


No comments:

Post a Comment