Rais John Magufuli amewasamehe wafanyakazi tisa wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), waliosimamishwa kazi kwa kosa la kutangaza habari ya uongo iliyomhusu. Wafanyakazi hao waliosimamishwa Machi 14, walirusha taarifa kwenye Televisheni ya TBC ikidai kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amesifu utendaji wa Rais Magufuli hasa vita dhidi ya dawa za kulevya ilhali siyo kweli.
Taarifa hiyo ambayo ilirushwa Machi 10, inadaiwa ilikuwa imeandikwa kwenye tovuti ya Fox Channel.com. Hata hivyo, baadaye iligundulika tovuti hiyo haikuwa ya Fox na kwamba, taarifa iliyokuwa imeandikwa ni ya uongo.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa TBC, Dk Ayub Rioba aliwasimamisha kazi wafanyakazi hao waliohusika na uandaaji na utangazaji wa habari hiyo. Hata hivyo, Rais Magufuli ambaye jana alifanya ziara ya kushtukiza ofisi za TBC pamoja na mambo mengine alitoa msamaha kwa wafanyakazi hao. Baada ya kufika alitembelea chumba cha kurushia matangazo na chumba cha habari na kukalia kiti cha watangazaji, huku akiigiza kama mtangazaji wa habari, alitumia fursa hiyo kuzungumza na wafanyakazi.
Akizungumza kwa njia ya simu, Dk Rioba alisema Rais alifika katika ofisi hizo kwa lengo la kuwatembelea na kuzungumza na wafanyakazi, kisha alitoa msamaha huo. Aliwataja waliosamehewa kuwa ni Gabriel Zackaria, Elizabeth Mramba, Prudence Constantine, Dorothy Mmari, Ramadhani Mpenda, Leya Mushi, Alpha Wawa, Chunga Ruza na Judica Losai.
No comments:
Post a Comment