Ile ndoto ya kiungo wa Yanga, Simon Happygod Msuva ya kutaka kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, inaweza kukamilika sasa baada ya uongozi wa timu hiyo kuweka wazi kuwa maongezi baina yao na timu ya Difaa El Jadida ya Morocco yamefikia kwenye hatua nzuri.
Wamorocco hao wanaiwinda kwa udi na uvumba saini ya Msuva aliyefunga mabao 14 katika msimu uliopita ambapo awali walikuwa tayari kumlipa dola 4,000 (karibu milioni tisa) kama sehemu ya mshahara wake.
Akizungumza kupitia Kipindi cha Spoti Hausi kinachorushwa na Globaltv Online, Kaimu Mkuu wa Kitendo cha Habari cha Yanga, Godlisten Anderson ‘Chicharito’, amesema kuwa wao kama uongozi wa Yanga wanaendelea ambapo kuna asilimia 85 za Msuva kuondoka ndani ya kikosi hicho.
“Ndani ya muda mfupi kila kitu kuhusiana na suala la Msuva kwenda Morocco kitakuwa wazi ambapo kwa sasa viongozi wanaendelea kulishughulikia kuhakikisha Msuva anaenda kukipiga nchini humo.
“Kuna asilimia 85 ya yeye kuondoka na tayari tumeshawaandaa baadhi ya wachezaji kuziba pengo lake pale atakapoondoka ambapo kuna wachezaji kama Juma Mahadhi wanaweza kuziba nafasi yake pale atapoondoka,” alisema Chicharito.
Msuva kwa sasa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuendelea kuitumikia Yanga ambayo inanolewa na Mzambia, George Lwandamina.
No comments:
Post a Comment