SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutakiwa kutimiza ahadi
yake ya kuweka vifaa vya kupima wabunge kama wametumia kilevi ama dawa
za kulevya kabla ya kuingia Ukumbi wa Bunge, amesema Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda ni mtani wake, hivyo watu wasijali maneno
yake.
Juzi Makonda alimwomba Spika Ndugai kuweka kipimo hicho ili kabla
wabunge hawajasimama kuchangia hoja wabainike kama wanatumia dawa za
kulevya au la.
“Kaka yangu Ndugai alisema ana nia ya kuweka kifaa maalumu kuwapima
wabunge kama wanatumia dawa za kulevya au la, hivyo atimize nia yake
hiyo ili kama na huko wapo tuwanyofoe,” alisema Makonda.
Akizungumza kwa simu, Ndugai alisema: “Makonda ni mtani wangu, mimi ni
Mgogo yeye ni Msukuma, kwahiyo tunataniana… msijali maneno yake,
alikuwa ananichapa tu kidogo.”
Wakati wa mkutano wa tatu wa Bunge la 11 Mei mwaka jana, Spika Ndugai
alipata kulieleza Bunge kuwa anafikiria kuweka vifaa maalumu vya kupima
ulevi kwa wabunge.
Ndugai alitoa kauli hiyo siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli
kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.
Alisema kuwa kuna wabunge kadhaa huingia bungeni wakiwa wametumia vilevi vikali.
“Tunajaribu ku-identify (kuwatambua) watu maalumu wanaoweza kutusaidia
kuzungumza na hawa watu ili waondokane na matatizo yale ambayo tutaweza
kuyagundua.
“Lakini wale wanaofanya kwa kificho itakuwa tabu kidogo. Lakini huko
mbele tutakwenda kwenye vifaa, maana si ulevi tu, kuna sigara kubwa
(bangi), unga (dawa za kulevya)… watu wanapiga konyagi hadi mchana,
kimsingi mambo ni mengi.
“Simaanishi wabunge wote, maana mtu anaweza kufikiri ni wote, hapana.
Hili ni kundi dogo mno la wabunge na hawajai hata mkononi. Lakini
wabunge walio wengi ni wazuri sana, hawanywi pombe wala nini. Kikundi
hiki kinahitaji msaada wa ushauri,” alisema Ndugai.
MAONI YA WABUNGE
Kauli ya Makonda ya kuwataka wabunge kupimwa akili ili kubaini kama
wanatumia aina yoyote ya dawa za kulevya au la, imepokewa tofauti na
baadhi ya wabunge.
Akitoa maoni jana kwa simu, Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema),
alisema wabunge tayari wameshapimwa akili na wananchi wao na ndio
maana wakapewa ridhaa ya kuwaongoza.
Alisema kulikuwa na michakato mingi hadi wao kuchaguliwa, ikiwa ni
pamoja na ya ndani ya chama, majimboni na hata kwenye Tume ya Uchaguzi
ya Taifa (NEC), hivyo wao wako safi hadi wakapitishwa na wananchi wao.
“Anayetakiwa kupimwa akili kama anatumia dawa au la au kama aliugua au
la ni mtu ambaye aliwahi kumfunga viatu mtoto wa rais, kulala kwenye
sebule ya Sitta, na hata kumpiga mzee Warioba na kutukana waliomzidi
umri bila sababu,” alisema Kubenea.
Aliongeza kuwa anaamini kwa wasiopimwa sehemu yoyote akiwemo Mkuu wa
Mkoa na wateule wengine wa rais ndio ambao wanatakiwa kupimwa.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu,
alisema Bunge ni mhimili mwingine, hivyo Makonda hana nguvu ya kuwataka
wao kupima.
Alisema kama ni mawazo ya kutakiwa kupima au kutopimwa, anayetakiwa
kusema hiyo ni Spika wa Bunge Ndugai na kama yeye ataafiki wao
watakubali kupimwa.
“Sisi mhimili wetu unasimamiwa na Spika ndiye mkuu wetu, lakini
alishawahi kusema hilo siku nyingi kwamba mhimili wake usiingiliwe
hovyo hovyo, lakini mtu mmoja mdogo sana anajiongelesha, ambaye hana
hata mamlaka,” alisema Sugu.
Alisema yeye mwenyewe Makonda ana matatizo yake na kama akihitaji wao wapimwe, watatakiwa kwenda wote.
Hata hivyo, Sugu ambaye ni Waziri Kivuli wa Habari Utamaduni na Sanaa,
aliwalalamikia waandishi wa habari kwa kumpa nafasi Makonda na kuacha
kuandika maoni wanayotoa wao kama wazo lake alilotoa bungeni siku ya
kufunga Bunge.
Mbunge huyo alisema anatamani siku moja Makonda apelekwe Mkoa wa Mbeya
na akawaongoze kwa miezi sita tu aone na si kukaa Dar es Salaam peke
yake huku akiingilia kazi za Spika.
Sugu alisema Serikali ya awamu ya tano inaonyesha wazi kwamba inalichukia Bunge kutokana na matamshi mbalimbali yanayotolewa.
No comments:
Post a Comment