Diwani wa Kata ya Mipingo, Saidi Naomari, aliwataja waliofariki dunia
katika tukio hilo kuwa ni Abdulrahman Mtopwa, Zainabu Nangungwa, Nuru
Machungira na Khadija Machungira, wakazi wa kijiji cha Namkongo.
Katika siku hiyo, Juma Mbilinga na Mohamed Limuhu wa kijiji cha
Mnyangara, na Swabaha Ahamad na mkewe Somoe Myemba wa kijiji cha Matapwa
walinusurika kwa kupanda juu ya mti na baadaye kuokolewa na majirani.
Diwani huyo alisema miili ya watu watatu ilipatikana na kuzikwa, na
kwamba mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa zimesababisha mito na
mabonde kujaa maji.
Naomari alisema mvua hizo licha ya kusababisha vifo, pia zimeleta hasara
kwa kusomba mifugo, kuharibu mazao mashambani, kubomoa nyumba na
kuharibu miundombinu ya mawasiliano ya barabara kati ya kata hizo na
maeneo mengine.
“Bado tathmini kamili ya mazao yaliyoharibiwa haijafanyika, lakini mbuzi
saba kati ya 30 wa Mohamed Limuhu, walisombwa na maji,” alisema Diwani
Naomari.
Alisema mawasiliano ya barabara kutoka Mipingo kwenda Mkwajuni na maeneo
mengine ya Vijiji vya Nangoo, Mnyangara na maeneo mengine, yamekosekana
kutokana na mvua hizo kubomoa madaraja na makalavati.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, alithibitisha kutokea kwa matukio na vifo hivyo.
Ndemanga alisema serikali ya wilaya ikishirikiana na mkoa, inaendelea na
utaratibu kwa ajili ya kuwasaidia waliokumbwa na majanga hayo.
No comments:
Post a Comment