Wapiga kura wanne wa Jimbo la Bunda waliofungua shauri kupinga
matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita wameendelea kumng’ang’ania mbunge wa
jimbo hilo, Ester Bulaya kwa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu
wa kutupa maombi yao.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe alisema
Jumatano hii kuwa rufaa ya wapiga kura hao, Magambo Masato, Matwiga
Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila iliyosajiliwa kwa namba 199 ya
mwaka 2016, itasikilizwa mfululizo kuanzia Februari 20.
Alisema rufaa hiyo itasikilizwa jijini Mwanza na jopo la majaji
watatu wa Mahakama ya Rufani, Salim Mbarouk, Augustine Mwarija na
Shabani Lila.
Katika maombi ya msingi waliyofungua Mahakama Kuu, wapigakura hao
wanaowakilishwa na Wakili Constantine Mutalemwa, wanaiomba Mahakama
kutengua ushindi wa Bulaya dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen
Wasira kwa madai kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka 2015 haukuwa huru na
wa haki.
Pamoja na madai mengine, Masato na wenzake wanadai kuwa mchakato wa
kampeni, upigaji kura na utangazaji wa matokeo uligubikwa na ukiukwaji
wa sheria na utaratibu wa uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa,
msimamizi wa uchaguzi kumnyima haki Wasira kwa kukataa ombi lake la kura
kuhesabiwa upya.
Novemba 17, mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu alimtangaza
Bulaya kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo baada ya kutupilia mbali
maombi ya wapigakura hao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment