Thursday 9 March 2017

KIZAAZAA MAITI YATOWEKA HOSIPITAL YA KCMC



FAMILIA ya marehemu Frank Mongi (56) aliyekuwa mtunza mifugo, imejikuta katika wakati mgumu baada ya kufika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuchukua mwili wa ndugu yao na kuukosa.

Baada ya kutafuta mwili huo kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa zaidi ya saa nane , ndugu hao walipewa taarifa kuwa mwili wa ndugu yao ulichukuliwa na familia nyingine na umeshazikwa tangu Machi 3, mwaka huu huko Mwanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema amepata taarifa hizo kutoka KCMC na amemuagiza Mkuu wa Kitengo cha upelelezi aende kufuatilia.

Akizungumzia tukio hilo, ndugu wa marehemu, Roman Mongi alisema Machi 2, mwaka huu walipeleka mwili wa Frank (kaka yake) baada ya kumkuta amefariki chumbani kwake katika eneo la Uchira alikokuwa anafanya kazi za kutunza mifugo.

Alisema juzi walifika hospitali na kulipa gharama zote ikiwemo ya kusafisha mwili, kwa sababu mwili wa kaka yake ulikuwa umeanza kuharibika, na kuahidi kwenda kuuchukua kesho yake.

Aliendelea kusema, jana saa moja asubuhi walifika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kwa ajili ya kuchukua maiti lakini hawakuiona, waliutafuta mwili hadi saa nane mchana, lakini hawakuuona, waliangalia maiti zote pamoja na orodha ya maiti zilizotolewa bila mafanikio.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Giliard Masenga, alisema kuna kosa la kiutendaji limetokea na mwili wa Mongi ulichukuliwa kimakosa na ndugu wa marehemu Ibrahim Msuya.

Alisema, Machi 3 mwaka huu, ndugu wa Msuya walifika hospitali na kuchukua mwili wa Mongi badala ya Ibrahim na kwenda kuuzika Mwanga lakini wamewasiliana na jeshi la polisi kwa ajili ya kwenda kuufukua mwili huo.

Alisema waligundua tatizo hilo baada ya orodha ya maiti zilizotolewa jana kuonesha mwili wa Msuya umechukuliwa, lakini bado upo kwenye chumba cha maiti. Awali, Roman alisema taratibu za mazishi ya Mongi zilikuwa zimeshafanyika huko Samanga, Marangu, ikiwemo kuchimba kaburi na Mchungaji alikuwa ameshafika.

Alisema kwa mujibu wa mila za kwao, hawawezi kufukia kaburi, hivyo kama mwili hautapatikana itabidi wachinje Kondoo, watupie utumbo na kisha waufukie. Aliongeza kuwa kaka yake alikutwa amekufa katika nyumba aliyokuwa akiishi na mwili wake ulikuwa umeanza kuharibika hasa upande aliokuwa amelala.


No comments:

Post a Comment