Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ametengua uteuzi wa wakurugenzi sita kwa mara nyingine.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya inasema uamuzi huo umefikiwa kutokana na
viongozi hao kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutohudhuria mkutano
wa kamati ya utendaji, licha ya kupelekewa taarifa.
Ilielezwa kuwa Profesa Lipumba Februari 17, alimuagiza Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho, Magdalena Sakaya kuwapa taarifa ya mkutano wa kamati ya
utendaji uliofanyika Februari 18 na walipelekewa mwaliko kwa posta.
Wakurugenzi waliotenguliwa na nafasi zao kwenye mabano ni Omar Ali Shehe
(Mipango na Uchaguzi); Salim Abdallah Bimani (Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Mawasiliano na Umma);
Abdallah Bakar Hassan, (Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi); Pavu Juma
Abdallah (Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria); Yusuf Salim
(Naibu Katibu Kamati ya Ulinzi na Usalama) na Mahmoud Ali Mahinda
(Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana).
Akizungumzia uamuzi huo, Bimani alisema hawamtambui Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho.
“Lipumba anafahamu kama alifukuzwa uanachama ndiyo maana alikata rufaa kupinga uamuzi wa mkutano mkuu,” alisema Bimani.
No comments:
Post a Comment