Aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Adam Malima amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka la shambulio.
Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai kuwa Mei 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi Malima alimzuia Ofisa wa polisi H.7818 PC ABDU kufanya kazi yake halali.
Malima ambaye alikuwa mbunge wa Mkuranga amedaiwa kumzuia Ofisa huyo kufanya kazi yake ya kumkamata Ramadhani Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph.
Kwa upande wa mshtakiwa wa kwanza, Ramadhani Mohammed Kigwande naye anakabiliwa na shtaka la kushambulia Mwita Joseph.
Wakili Kombakono aliendelea kudai kuwa Mei 15,2017 kwenye eneo hilo la Masaki wilaya ya Kinondoni mshtakiwa huyo akiwa na nia ya kumzuia Mwita Joseph ambaye ni Ofisa oparesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises wakati alipokuwa akimkamata kwa kupaki vibaya gari namba T 587 DDL alimshambulia(Mwita) na kumsababishia maumivu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo,washtakiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Mkazi Mkuu,Respicius Mwijage alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh 5milioni.
Washtakiwa wamekamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa huru.
Washtakiwa wanatetewa na wakili Peter Kibatala ambaye amewasilisha pingamizi dhidi ya shtaka la pili kuwa shtaka halifanani na maelezo ya kosa.
Hakimu Mwijage ameiahirisha kesi hiyo namba 168 ya 2017 hadi Juni 15,2017 kwa ajili ya kutajwa ambapo pia pingamizi hilo litasikilizwa.
No comments:
Post a Comment