Thursday, 4 May 2017

Sakata la Makonda kuivamia Clouds laibuliwa na kuja na sura mpya sasa ndani ya mahakama kujieleza



SAKATA la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds liliibuliwa upya na wadau wa habari jana baada ya kulilaani.


Wadau hao wa habari walilaani tukio hilo jana ikiwa ni siku maalum ya Uhuru wa Habari iadhimishwayo Mei 3 kila mwaka.


Akizungumza kama mgeni rasmi katika siku hiyo jijini, Mbunge wa viti maalum wa Chama Cha Wananchi (CUF), mkoa wa Dar es Salaam, Salma Mwasa alisema si jambo jema viongozi wa umma kuonekana wanakuwa mstari wa mbele kuminya uhuru wa habari.


Alisema kitendo alichokifanya mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam ni cha kulaaniwa na kitaendelea kulaaniwa na kila mpenda amani na mpenda ustawi wa vyombo vya habari, na anayetambua umuhimu wake katika nchi.


“Viongozi wa umma na watunga sera, wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda vyombo hivi vya habari na kuhakikisha vinafanya kazi yao kwa uhuru," alisema Mwasa.


"(Viongozi wa umma) wanapogeuka na kuonyesha wa kwanza kuviminya (vyombo vya habari) inaonyesha sifa mbaya na hawapeleki ujumbe mzuri kwa hawa wengine wanaowategemea, wanaowasikiliza na kuwaamini.


“Kiukweli kile kitendo kinatakiwa kulaaniwa na kitaendelea kulaaniwa, kwa sababu pasipo kufanya hivi, vitendo hivi vinaweza kuendelea kufanyika na huko tunakoenda hali ya uhuru wa vyombo hivyo inaweza ukawa mgumu zaidi.”


Tukio hilo la staili ya utekaji wa vituo vya habari wakati wa mapinduzi ya kijeshi, lilifanywa na mkuu huyo Machi 17 saa 5 usiku.


Mkuu huyo alionekana katika video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii akiwa na askari wasielekea kuwa polisi, waliokuwa na bunduki.


Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya waziri iliyochunguza sakata hilo, mkuu huyo alivamia kituo hicho usiku huku vipindi vikiwa vinaendelea na kwamba aliwatisha na kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kuonyesha taarifa yake.


Taarifa hiyo ya upande mmoja, ilikuwa ikimtuhumu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuwa amezaa na muumini wake.


Gwajima ambaye alikanusha vikali madai hayo kanisani kwake, alianzisha tuhuma za mkuu huyo kutumia cheti feki kujiunga na elimu ya juu na kwamba jina lake halisi ni Daud Bashite.


Mwasa alisema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini inazidi kuwa mbaya kadri siku zinavyosonga na kwamba licha ya changamoto wanazokutana nazo, waandishi wa habari hawapaswi kukata tamaa.


“Tumeshuhudia baadhi ya waandishi wanapigwa na wengine hata kujeruhiwa wanapokuwa wanafanya kazi zao," alisema Mwasa. "Nataka kuwaomba wasikate tamaa."


"Watanzania wanawategemea, wakumbuke kuwa hakuna ukombozi bila mateso, tunajua wako katika wakati mgumu lakini tunaomba hali hiyo isiwakatishe tamaa.”


Alisema wao kama wawakilishi wa wananchi, wataendelea kupambana kuhakikisha uhuru huo unalindwa hata ikiwezekana kujenga hoja bungeni ili Sheria ya Vyombo vya Habari iliyopitishwa hivi karibuni irudishwe bungeni ili baadhi ya vipengele ambavyo vilionekana kuwa vina mtego kwa waandishi hao, virekebishwe.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Siasa (Taporea), George Maziku alisema ripoti ya hali ya uhuru wa waandishi wa habari iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka inaonyesha kuwa katika miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi 800 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameuawa wakiwa wanatekeleza majukumu yao.


Akizungumzia Sakata la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni, alisema ni jambo la kusikitisha kuona mpaka sasa hakuna hatua yoyote ambayo mkuu huyo amechukuliwa.


No comments:

Post a Comment