KARIBU wabunge 200 wa Democrats wamesema watafungua mashitaka dhidi ya Rais Donald Trump wakidai kuwa kuendelea kwake kujihusisha na biashara zake kunakiuka Katiba ya nchi.
Mashitaka hayo yatamtuhumu Trump kwa kukiuka Kifungu cha Maslahi cha Katiba ya Marekani, ambacho kinakataza maofisa wa Serikali kupokea zawadi au wadhifa kutoka serikali za kigeni bila kuidhinishwa na Bunge, kwa mujibu wa wabunge wanaoongoza azma hiyo.
Kesi hiyo itakuwa na walalamikaji wengi kuliko kesi yoyote iliyopata kufunguliwa dhidi ya Rais katika historia ya Taifa hili, kwa mujibu wa Mbunge wa Michigan, John Conyers, ambaye yuko kwenye Kamati ya Bunge ya Sheria.
“Hatufanyi hivi kujifurahisha au kupendelea, lakini ni kwa kuwa Rais Trump ametufanya tushindwe kufanya vinginevyo,” alisema.
Shirika la Trump linajumuisha zaidi ya kampuni 500 za kibiashara zilizo kwenye takriban mataifa 20 duniani, na zinahusisha hoteli, viwanja vya gofu na nyumba za makazi, nyingi zikifanya biashara na serikali za kigeni.
Serikali hizo zimelipia matukio mbalimbali kwenye hoteli za Trump na ada za matengenezo ya vyumba katika majengo ya Trump.
Ingawa Shirika la Trump limeahidi kutoa faida zitokazo kwenye Serikali hizo katika biashara ya hoteli kwa ajili ya Hazina ya Marekani, waraka wa sera za kampuni uliotolewa mwezi jana, unaonesha kuwa mali za Trump hazitathibitisha kama wateja binafsi ni wawakilishi wa serikali za kigeni kibiashara.
Seneta Richard Blumenthal wa Connecticut, alisema mashitaka hayo ni ya lazima ili kumlazimisha Trump aweke hadharani ni kwa kiasi gani kampuni zake zinaendesha biashara na serikali za kigeni na kuruhusu Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kutoa au kutotoa ruhusa chini ya Kifungu cha Maslahi.
“Hatuwezi kuruhusu tusichokijua,” alisema. “Anaingilia wajibu wetu wa kikatiba.”
Trump na wanasheria wake wamesema kifungu hicho hakihusiki na miamala ya soko la haki na kwamba alishachukua hatua za kujiondoa kwenye biashara zake.
Hata hivyo, wakfu ambamo Trump amewekeza mali zake unaendeshwa na wanawe wa kiume. Trump ni mnufaika pekee wa wakfu huo na anaweza kuchukua fedha muda wowote atakao.
Anatarajiwa kupokea taarifa za fedha za biashara yake wakati wote akiwa madarakani. Ni rais pekee katika historia ambaye hajawasilisha nakala ya marejesho yake ya kodi.
Wabunge hao walisema watawasilisha malalamiko yao Jumatano asubuhi kwenye Mahakama ya Wilaya ya Marekani ya Washington DC. Kesi hiyo inataka uamuzi wa Mahakama unaosema Trump anahusika na Kifungu cha Maslahi na amri ya kumtaka Trump asipokee zawadi.
Wabunge hao wanawakilishwa na Kituo cha Uwajibikaji Kikatiba, kilichoko DC ambacho ni cha kisheria “kilichopo kwa ajili ya kukidhi utekelezaji wa Katiba.”
Kutokana na kutofautiana kwa kanuni za kimaadili za Bunge na Baraza la Seneti, maseneta watatenganisha gharama za uwakilishi wa kisheria. Kituo hicho cha Uwajibikaji Kikatiba kitatoa huduma za kisheria kwa wabunge hao.
No comments:
Post a Comment