Wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka ngazi ya
shina, tawi, wilaya na mkoa wapatao 1,520 wamefukuzwa uanachama kwa
makosa ya kukisaliti chama kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Taarifa iliyolifikia gazeti hili juzi ilieleza kuwa miongoni mwa
waliofukuzwa ni pamoja na viongozi wa ngazi za wilaya, mkoa na taifa
ambao ni tisa akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) Wilaya ya
kichama ya Meru, Julius Mungure, na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha,
Dk Wilfred Soilel.
Akizungumza jana jijini hapa na waandishi wa habari kutoka vyombo
mbalimbali, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Omari Billaly, alisema
uamuzi ya NEC Mkoa iliyokutana Februari 11 mwaka huu kuhusu
waliokisaliti chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
Billaly alisema Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Arusha imetimiza wajibu
wake kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Ibara ya 93 (14).
Alisema halmashauri hiyo imeamua kuwafukuza uanachama wanachama hao
baada ya kupatikana na makosa ya kukisaliti chama kwenye uchaguzi huo
mkuu wa madiwani, wabunge na rais.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi na maadili za CCM toleo la
2012 fungu la nane ibara ya 8(IX)(a) inajieleza wazi kuwa kosa kubwa
kuliko yote katika CCM ni kukisaliti chama na kukiweka katika hali ya
kushindwa katika uchaguzi wa dola.
Alisema lengo la chama cha siasa ni kushika dola kwa hiyo kiongozi au
mwanachama yeyote anayethibitika kukisaliti chama adhabu yake kwa
mujibu wa kanuni hizi ni kufukuzwa uanachama.
Wengine waliofukuzwa ambao ni viongozi ni Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana (UVCCM) Wilaya ya Karatu na diwani wa Viti Maalum, Bibiana
Nanyaro, na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya na Mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa Taifa, William Sarakikya.
Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM, Meru Aziza
Mundo, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Wilaya ya Arumeru Evaline
Nanjway na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi Wilaya ya Arumeru,
Salome Samwel.
Source: Habari Leo
No comments:
Post a Comment